Mbunge ajiuzulu baada ya kuiba mkate

Muktasari:

Spika wa Bunge amkosoa vikali akisema ametenda kosa lisilokubalika

 


Slovania. Mbunge nchini Slovenia, Darij Krajcic amejiuzulu baada ya kuiba mkate dukani.

Aliiba mkate huo kwa madai kuwa wahudumu walimpuuzia kwani wakati akihitaji kununua mkate, waliendelea na shughuli zao.

Haikujulikana kama ameiba lakini baadaye baadhi ya watu walisisitiza arudi kulipa fedha ya mkate huo.

Krajcic ameomba msamaha na kusema kuwa anajutia kitendo alichokifanya.

Suala lake la kuiba lilisambaa baada ya kuwaambia wabunge wengine wakati wa mkutano wa kamati siku ya Jumatano.

''Nilisimama pale kwa dakika tatu lakini hawakunihudumia,” amesema mbunge huyo wakati akizungumza na kituo kimoja cha televisheni.

Wafanyakazi watatu wa duka hilo hawakugundua kama mbunge huyo alikuwepo katika duka hilo kutokana na kuwa katika mazungumzo.

''Hakuna mtu yoyote aliyepiga kelele, wala kunifuata,” amesisitiza mbunge huyo ambaye amechekwa na wabunge wenzake waliposikia kisa hicho.

Jana Alhamisi  Februari 14, 2019, Spika wa Bunge la nchi hiyo, Brane Golubovic, alikemea vikali kitendo cha mbunge kuiba na kusema ni jambo lisilokubalika.

''Amechukua hatua za kuwajibika na kujiuzulu yeye mwenyewe," Golubovic aliviambia vyombo vya habari.