'Niliuza nywele zangu kwa $2 ili watoto wangu 3 wapate chakula

Prema na kijana wake
Maelezo ya picha, Prema alikuwa na wakati mgumu kupata chakula cha watoto wake baada ya mume wake kujiua lakini kunyoa nywele zake kukawa mkombozi wa muda.

"Kijana wangu wa miaka 7 Kaliyappan alikuja kutoka shuleni na kuomba chakula. Kisha kaanza kulia kwasababu ya njaa," amesema Prema Selvam.

Lakini mama yake mwenye umri wa miaka 31, ambaye anaishi eneo la Salem mji wa Tamil Nadu, nchini India, hakuwa na chochote cha kumpa na alihisi kukosa matumaini kabisa.

Nini hasa kilichotokea, Ijumaa Januari 3. Hakuwa na chochote cha kupika.

Baada ya siku kadhaa za matukio kama hayo, Prema alikuwa amefikia kiwango kibaya na kuamua kuchukua hatua ambayo haikuwa ya kawaida na watu wengi wa jamii yake wakaitikia wito.

'Nilivunjika Moyo'

Kumuona kijana wake mkubwa Kaliyappan (aliyevaa fulana nyekundu) njaa kulimpa Prema uchungu mwingi sana
Maelezo ya picha, Kumuona kijana wake mkubwa Kaliyappan (aliyevaa fulana nyekundu) njaa kulimpa Prema uchungu mwingi sana

"Sikuwa na chochote cha kuipa familia yangu. Nilisikita sana. Na nikaanza kufikiria kuna haja gani ya kuishi wakati siwezi kulisha watoto wangu?" aliiambia BBC.

Prema hakuwa na mali, vito vya thamani, ama hata vyombo vya nyumbani ambavyo vingeweza kubadilishwa kwa pesa.

"Sikuwa hata na noti ya rupia 10 (senti 14)," amesema. "Nilikuwa na ndoo ndogo tu za plastiki."

Kisha akagundua kwamba kuna kitu anachoweza kuuza.

Kuuza nywele kulingana na uzito wake

Muumini wa Kihindu Rani, alinyoa nywele zake katika hekalu nchini India.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Muumini wa Kihindu Rani, alinyoa nywele zake katika hekalu nchini India. Alikuwa anatoa nywele hizo akimuomba Mungu amumpe mjukuu.

"Nilikumbuka duka ambalo nilikuwa nikinunua nywele. Nilienda hapo na kuuza nywele zangu zote kichwani kwa rupia 150 ($2)," Prema amesema.

Nywele za kubandika za binadamu huuzwa kote ulimwenguni na India ndiyo inayouza kiwango cha juu cha nywele hizo nje ya nchi.

Baadhi ya waumini wa kihindi hutoa nywele zao kwenye mahekalu baada ya kujibiwa maombi yao.

Wanaohusika na biashara hiyo hununua nywele hizo na kuziuza nje ya nchi.

Maamuzi ya mumewe ya kujiua

Prema
Maelezo ya picha, Mipango ya serikali ya kusaidia maskini nchini India mara nyingi hushindwa kufikia walengwa kama Prema

Kiwango cha pesa alichopata kinaweza kununua chakula katika migahawa ya watu wa tabaka la kati kwenye mji anaoshi. Lakini kijijini mwao alifanikiwa kununua zaidi.

"Niliweza kununua vifungashio vitatu vya wali kwa gharama ya rupee 20 (senti 28) kwa watoto wangu watatu," amesema.

Akala chakula hicho na watoto wake na kupata afueni ya muda tu.

Prema alijua kwamba hana tena njia yoyote ya kupata pesa na kuanza kuwa na wasiwasi kuhusu vile atakavyo hakikisha familia yake imepata chakula.

kwa miaka mingi alikuwa akifanya kazi na mume wake ya utengenezaji wa matofali na walikuwa wakipata kile kidogo cha kukimu mahitaji yao.

Mume wake alikuwa amechukua mkopo kuanza biashara hiyo ya kutengeneza matofali lakini mambo hayakwenda kama walivyopanga na huo ndo ulikuwa mwanzo wa kero za maisha na msongo wa mawazo.

Hakuweza kupata pesa za kutosha na kujipata akiwa katika hali ya kukatisha tamaa.

Miezi saba iliyopita, muwewe, alishindwa na maisha, akakata tamaa na kuamua kujiua kwa kujichoma moto.

Baada ya kuuza nywele zake, na bila ya kuwa na mtu wa kumtegemea, Prema alitaka kufuata nyao za mumewe na kujaribu kujiua vilevile.

Prema alijaribu kujiua

"Nilikwenda dukani na kuulizia dawa ya kuua wadudu."

Lakini muuzaji alipomuona akiwa katika hali ya kusononesha, muuza duka akamfukuza.

Alipofika nyumbani akaamua kujaribu njia nyengine na kuanza kuchuma mmea wa manjano wa oleander, kisha akausaga ili uwe rojo rojo.

Kwa bahati nzuri, dadake ambaye ni jirani, akaingia na kuanza kumuomba asile mmea huo kwasababu ni sumu.

Prema anasema shinikizo ya kurejesha pesa zilizokopwa na mumewe ilikuwa zimefika mwisho.

Kufanya kazi ngumu

Prema with two of her kids
Maelezo ya picha, Kuuza nywele zake kulimfanya Prema apate pesa za haraka

Prema ndo mtafutaji pekee wa riziki kwa familia hiyo baada ya mumewe kujiuwa. Bado anafanya kazi ya kutengeneza matofali ambayo ni ngumu lakini yenye kipato cha juu ikilinganishwa na kibarua cha kulima.

"Ninapokwenda kufanya kazi napata rupee 200 ($2.80) kwa siku, ambayo inanitosha kwa ajili ya familia yangu," anasema Prema.

Kawaida anapokwenda kufanya kazi huandamana na watoto wake wawili kwasababu hawajafikisha umri wa kuanza shule.

Lakini katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya kuuza nywele zake, mara nyingi alikuwa mgonjwa, na hivyo kumaanisha kwamba hakuweza kupata kipato kama alivyotarajia.

"Sikuweza kubeba matofali yenye uzito mkubwa. Na wakati mwingi nilikuwa nyumbani kwasababu ya homa."

Mikopo iliyolimbikizana

Prema alianza kukosa kulipa mikopo. Na wakati wakopeshaji wake walianza kudai tena nguvu, matatizo yake yakaongezeka.

Hakusoma na hakujua lolote kuhusu miradi ya serikali ya kusaidia watu maskini kama yeye.

Mfumo wa kawaida wa benki nchini India una sheria kali na kufanya iwe vigumu kwa jamii maskini kupata mikopo kwa riba ya chini.

Prema na mume wake walikuwa wameomba pesa kutoka kwa wakopeshaji wa eneo na majirani.

Lakini kwasababu mikopo hii haina wadhamini gharama yake iko juu.

Kila Prema alipokuwa mgonjwa, alikuwa akipokea pesa kidogo na kumuacha kuwa katika hali ya kukata tamaa.

Ilipofikia wakati huu, akaamua kuuza nywele zake na mambo yalipozidi unga akaamua kujiua.