Mkate wa kombamwiko ulio na protini nyingi zaidi ya nyama, lakini je unaweza kuula?

Cockroach bread

Chanzo cha picha, FURG

Maelezo ya picha, Watafiti wanasema mkate huo hauna tofuati kubwa kwa ladha na mikate ya kawaida

Tazama mkate huu kwenye picha. Bila shaka unakaa kama mkate mwingine wowote wa kawaida.

Hatahivyo umepikwa kwa kombamwiko. Hasaa, umetumika unga uliotengenezwa kutokana na wadudu hao.

Watafiti wa vyakula Brazil walivumbua unga huu kama suluhu kwa tatizo la uhaba wa chakula duniani.

Na pia kwa kinacho kadiriwa kuwa ni kupungua kwa protini inayotokana na wanyama duniani katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu duniani.

Dried lobster cockroaches

Chanzo cha picha, FURG

Maelezo ya picha, Moja ya faida ya kutumia kombamwiko ni unafuu wa bei yake

Hesabu ya haraka

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, takriban watu bilioni 9.7 watakuwa duniani kufikia mwaka 2050.

Umoja wa mataifa unapendekeza watu waanze kula wadudu pakubwa katika chakula wanachokula - kutokana na kiwango cha juu cha protini walichonacho, na unafuu wa bei.

Tayari wadudu huliwa katika baadhi ya jamii katika maeneo tofuati duniani.

Lakini sio kombamwiko wale wanaozunguka katika mitaro na mabomba ya choo na maji taka waliotumika hapa. Watafiti Brazil wametumia aina fulani ya kombamwiko anayejulikana kama 'Lobster roach' asili yake ikiwa ni Afrika kaskazini.

Huliwa wakiwa hai na baadhi ya jamii zinazofuga buibui aina ya tarantula na hata mjusi.

Sliced bread

Chanzo cha picha, FURG

Maelezo ya picha, Mkate hutengenezwa kwa 10% ya unga wa wadudu

Wanazaana haraka na kwa urahisi.

Wadudu hao walichaguliwa kutengenezwa unga kwa sababu kadhaa: kando na kiwango kikubwa cha protini, mdudu huyo amekuwepo kwa mamilioni ya miaka - na amesalia alivyokuwa miaka ya nyuma ki jinia.

Mkate uliosheheni Protini

Wanasayansi Brazil wametengeneza unga huo kutokana na kombamwiko waliokauka ambao gharama yake ilikuwa ni $51 kwa kilo. Walisagwa ndani ya maabara.

Mkate huo hutengenezwa kwa 10% ya unga wa wadudu, na unga wa kawaida wa ngano.

"Unga wa kombamwiko uliongeza protini kwa 133% katika mkate" mwanasayansi Andressa ameiambia BBC .

Mkate wa kawaida wa gramu 100 ulikuwa na gramu 9.7 za protini, tofauti na mkate wa kombamwiko uliokuwa na gramu 22.6 za protini.

Andressa, ameeleza hakuna tofuati kubwa ya ladha kati ya aina hizo mbili za mkate.

Anadai kwamba kula wadudu kuna madhara kidogo kwa mazingira kuliko vyanzo vingine vya kawaida vya chakula.

Lobster roaches

Chanzo cha picha, FURG

Maelezo ya picha, Wanasayansi wanadai hakuna tofuati kubwa ya ladha kati ya aina hizo mbili za mkate

Kwa mujibu wa kampuni ya utafiti nchini Marekani, Global Market Insights, soko la wadudu wanaoliwa litakuwa na kupita thamani ya $ milioni 700 katika miaka mitano ijayo.

Kwa hivyo, upo tayari kula mkate wa kombamwiko?