May 6, 2024

Sababu za wanawake wa Tanzania kurudia nywele za asili

Nywele asilia umekuwa ndiyo mtindo mpya kwa wanawake kwa sasa. Baadhi ya saluni kutengeneza nywele kwa dawa zimeanza kukosa wateja.

  • Ni pamoja na uamuzi wa kuukubali uhalisia wao na kujivunia Uafrika.
  • Baadhi yao wamesema kwa kukaa na nywele asilia, wamefanikiwa kuokoa muda na gharama walizokuwa wakizitumia awali.
  • Matunzo ya nywele asilia, yamekuwa ni sababu kwa baadhi yao kushindwa kuagana na “Team natural”.

Dar es Salaam. Miaka kadhaa iliyopita, ilikuwa ni ngumu kidogo kumkuta binti wa Kiafrika hasa mijini akikatiza mitaani kwa mikogo katika majiji makubwa kama Dar es Salaam akiwa na nywele zake za asili. Wengi walipendelea nywele bandia za kushonea maarufu kwa Kiingereza ‘weaving’ huku wengine wakivalisha vichwa vyao mawigi ya mitindo tofauti.

Wanawake wachache kama wanamitindo Nancy Sumari na Flaviana Matata ndiyo waliweza kuuwakilisha uhaalisia wamwanamke wa kuafrika kwakuwa mara nyingi walionekana wakiwa na nywele fupi za asili. 

Wanawake wengi hasa mijini wanaeleza kuwa hupendelea kuweka dawa kwenye nywele zao ikiwa ni kujipatia urahisi wa kuzihudumia kama alivyosema Jessica Kimosso Mkazi wa Dar es Salaam.

Hata hivyo, hivi karibuni, idadi ya wanawake ambao wanatengeneza nywele zao katika mtindo wa nywele za asili inazidi kuongezeka wengi wakidai kuchoshwa na matumizi ya dawa za kulainisha nywele maarufu kama “relaxers” na kuchagua nywele asilia au kama wao wanavyoziita kwa kimombo “Natural hair”.

Huenda wewe ni miongoni mwa wanaonajiuliza ni kwa nini wanawake wameamua kufanya mapinduzi haya ya kimtindo na kurejea kwenye nywele za asilia zilizoonekana awali kupitwa na wakati?

Baadhi ya wanawake na wana mitindo wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) katika ripoti hii maalum kuwa kuna sababu lukuki za kuamua kubaki na nywele asilia zikiwemo muda, na unafuu wa gharama

Ilikuwa ni ngumu kidogo kumkuta binti wa Kiafrika hasa mijini akikatiza mitaani kwa mikogo katika majiji makubwa kama Dar es Salaam akiwa na nywele zake za asili. Picha| Addiah Natural and Beauty Bar.

Kuikubali asili yao

Mfanyabiashara wa mapambo na maua jijini Dar es Salaam Salama Masoud anasema nywele ni utambulisho wake maalum jambo lililomfanya kurudia kwenye nywele zake za asili kama mwanamke hasa baada ya nywele za dawa kutokumridhisha.

“Zamani nilikuwa naweka dawa ya nywele. Niliamua kuacha kwa sababu nywele zangu zilikuwa nyembamba sana na sikuzifurahia. Niligundua kuwa nywele zangu ni nzuri bila hata kuweka dawa. Nilianza kuangalia video kwenye mtandao wa YouTube jinsi navyoweza kuzitunza nywele zangu asilia na hakika nimefanikiwa,” anasema Salama.

Zaidi, binti huyo ameiambia Nukta Habari kuwa anachofurahia zaidi ni urahisi wa kuzihudumia nywele asili kwa kuwa unahitaji vitu ambavyo vipo nyumbani vikiwemo maparachichi na mayai na sio kemikali kama alizokuwa akizitumia awali.

Baadhi wanaotumia dawa zinazotumika kutengeneza nywele kuwa kama karikiti wanasema wamekuwa wakidai utunzaji wa nywele asilia ni ghali kuliko inavyodhaniwa.

Nywele asilia ni nafuu kuliko nyingine

Hata hivyo, Mkazi wa Sinza jijini  Dar es Salaam Nasikiwa Suzie anaeleza kuwa utunzaji wa nywele asilia hauusishi gharama kubwa kama ilivyo kwa wanaotumia relaxers. 

Kwa Nasikiwa, ambaye amesokota rasta (dread locks) amesema kwa mwezi anatumia wastani wa kati ya Sh10,000 hadi Sh20,000 kwa ajili ya nywele zake. Hapo ataenda saluni na kuzihudumia nywele zake ikiwemo kuziosha.

“Nikitumia zaidi ya hapo ujue nimenunua mafuta na huwa yanakaa kwa miezi mitatu,” anasema.

Huduma za nywele za asili pia zinatofuatiana gharama kutokana na maeneo wahusika wanapoenda kutengenezewa. Wengi wanaojitengeneza gharama zao huwa chini zaidi kuliko wanaoenda kwenye saluni za nywele. 

Hata wale wanaoenda saluni kiwango cha kutoboa mfuko nacho hutofautiana. Wanaoenda saluni za kawaida mitaani hulipa gharama ya chini kuliko wale wanaoenda kwenye saluni maarufu za nywele za asilia hususan kwenye majiji makubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar. 

Hata hivyo, gharama zao za juu huenda zisifikie hata asilimia 30 ya wale wanaonunua mawigi ya bei mbaya ambayo mengine huzidi hadi Sh700,000. 

Kwa ambao hawatengenezi nywele za asili gharama za chini ni kubwa kidogo kuliko wenzao. 

Watu wenye nyele zaasili wana uhuru zaidi na nywele zao. Picha| Haikasia Malle.

Wakati Nasikiwa akitumia chini ya Sh40,000 kila mwezi, Mbunifu wa picha na machapisho Evon Evance, ambaye hatunzi nywele zake asilia, anasema yeye hutumia hadi Sh 80,000 kwa mwezi kuhudumia kichwa chake.

Evon anasema gharama hiyo ni ya kununulia rasta zenye kiwango bora ili asukapo ziwe na uhalisia thabiti wa nywele zake.

“Ninatumia Sh80,000 kununua rasta kwa kuwa najisuka, gharama ya ususi ninaiepuka,” anasema Evon ambaye mbali na kiwango hicho, huingia gharama ya kununua mafuta ya nyele hizo (hair spray) kama sehemu ya huduma kwa nywele hizo. 

Hii ina maana kuwa iwapo angemtafuta na msusi kutengeneza nywele hizo huenda ingemtoka hata Sh100,000 ukijumlisha na nauli kwa wale wanaosafiri umbali mrefu kidogo kufuata huduma hiyo. 


Zinazohusiana


Nywele asilia zinatunza muda

Ni mara ngapi umewahi kumshuhudia mwanamke akiwa anatengeneza nywele wakati akitaka kutoka? Kama umewahi, basi utaelewa ni kwa nini wanawake huchelewa hata harusini au katika hafla mbalimbali. 

Baadhi ya wanawake wameniambia kuwa matumizi makubwa ya muda wakati wa kuandaa nywele zisizo za asili ni miongoni mwa sababu zinazofanya waachane nazo.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro, Emily Komba aliamua kukata nywele zake kutokana na kupoteza muda wakati akijiandaa. 

“Nilikuwa hadi nachelewa vipindi darasani. Ujue kama umeshonea weaving, usipojua kulitunza, unaweza ishia kunuka kichwa,” anasema Emily.

“Saa zingine unalazimika kufunga kiremba sasa usiombe weaving (nywele za kushonea) lianze kukuwasha. Kutoa kiremba darasani huwezi kwa sababu hujachana, unabaki unajipiga piga. Tangu nimenyoa, naamka, naoga, nachana nywele, naenda darasani,” Emily anasema. 

Fursa, maumivu kwa biashara ya urembo

Mtindo wa nywele asilia unazidi kuliteka soko na tayari madhara yake au faida zimeanza kuonekana kwenye biashara ya nywele na dawa zake. 

Muuzaji wa duka la bidhaa za urembo za jumla lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam Hatib Mgolongwa ameiambia Nukta kuwa kwa sasa bidhaa nyingi za kufanyia steaming na kuweka dawa kwenye saluni hazitoki kama ilivyokuwa awali. 

Mathalani, Hatib anasema zamani watu wengi walikuwa wakinunua dawa ya “easy wave” na “blow out” makopo madogo na kati na wengi walikuwa wauzaji wa maduka ya kawaida waliowauzia watu wanaojiwekea dawa nyumbani.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo anasema kwa sasa watu wanaonunua dawa hizo wamepungua na hata wanaonunua “steaming” wamepungua ikilinganishwa na zamani.

“Nilikuwa nauza steaming za brand moja hivi maarufu hata katoni mbili kwa siku lakini sasa hivi utakuta nauza pisi tano, tatu inategemea na siku. Ila zamani, mambo yalikuwa mazuri. Siku hizi nachouza kwa wingi ni shampoo. Hizi dumu za lita tano unazoziona, zinabebwa acha,” anasema Mgolongwa huku akionyesha madumu hayo na kuachia tabasamu kidogo ikilinganishwa na alivyokuwa akisimulia ukame wa mauzo kutoka kwenye dawa za nywele. 

Utokoaji wa shampoo siyo wa bahati mbaya. Bidhaa hiyo ni moja ya zile zinazotumiwa zaidi na watu wenye nywele za asili na hata wale wanaotumia nywele za dawa. 

                                         

Natural’ (asilia) ndiyo imekuwa ‘fashion’ (mtindo) kwa kuwa hata wanaoweka dawa, wanakwambia naziweka miezi mitatu baadaye nitazikata. Video| Addiah Natural and Beauty Bar.

Kwenye saluni, wateja wa kutengeneza nywele za dawa nako wameanza kupungua huku wale wa nywele asilai wakianza kuongezeka. Watoa huduma wanaotoa huduma zote kwa sasa ndiyo wanaokula bingo. 

Mtaalamu wa nywele kutoka saluni ya Zally Saloon iliyopo maeneo ya Airport jijini Dar es Salaam, Zainabu Gwazai anasema zamani walikuwa wakiweka dawa watu sita hadi 10 kwa siku na mambo yalikuwa mazuri zaidi siku za wikiendi.

“Siku hizi kwa mwezi tunaweza kuweka dawa mara mbili au mara tatu tu. ‘Natural’ (asilia) ndiyo imekuwa ‘fashion’ (mtindo) kwa kuwa hata wanaoweka dawa, wanakwambia naziweka miezi mitatu baadaye nitazikata,” anasema Zainabu.

Mwenendo huu umeshuhudiwa na wahudumu wengi wa saluni jijini hapa akiwemo Caren Hezron anayehudumu katika saluni ya Wealthy Style iliyopo Sinza  jijini Dar es Salaam.

Caren anasema miaka mitatu iliyopita wateja wa kuweka relaxers walikuwa ni wengi ikilinganishwa na sasa. Kwa wikiendi, Caren anasema hadi watu 16 walifika saluni kuweka dawa.

“Kwa sasa wamepungua sana mwaka juzi mwanzoni wallikuwa wengi wanaweka dawa lakini sasa hivi wengi wanahamia kwenye nywele asili,” anaeleza Caren ambaye saluni yao tayari ilishaona ujio wa fursa za nywele asilia miaka mitano iliyopita. 

Je, nywele asilia zinachagua baadhi ya vichwa? 

Licha ya kuwa urembo wa nywele asilia unavutia watu wengi, utunzaji wake huenda ikawa ni sababu  inayowakwamisha wengine kuungana na wanawake wenye  nyele asilia. Mbali  na sababu hiyo, wapo wanawake ambao nywele zao wanaziona haziridhishi ikiwa ni pamoja na ukuaji na kujaa kwa nywele kichwani.

“Niliweka kila kitu. Kila dawa ninayomudu nimetumia lakini nikikutolea hili wigi, utashangaa kuona “tunywele” “nilitonato,” amesema Regina Simon mkazi wa Arusha.

Unahitaji kujua ni nini Regina anaweza kufanya ili kufanikisha utengenezaji wa nywele za asili? 

Fuatilia sehemu ya pili ya makala haya kufahamu njia bora za kutunza nywele za kiafrika.