Kwa ugumu wa ajira kwa zama hizi na kwa matatizo yanahohusiana na ajira watu wengi wameanza kuangalia vipato tofauti na ajira. Na njia nzuri inayooneka ya kujipatia kipato tofauti na ajira ni kufanya biashara.

  Pamoja na biashara kuwa njia bora bado kuna watu wengi huku mitaani wanafanya biashara kwa miaka mingi ila hawana mabadiliko makubwa. Kuna watu wanafanya biashara moja kwa muda mrefu ila mabadiliko ni madogo sana kwenye maisha na biashara zao.

  Kuna watu wengi wanafanya biashara ila hawana tofauti na watu walioajiriwa, kwa sababu siku atakayoacha kwenda kwenye biashara yake adhari inakuwa kubwa sana. Yaani uwepo wake kwenye biashara yake ndio roho ya biashara hiyo.

            kuza biashara

  Kama unafanya biashara yako kwa muda mrefu ila unaona bado haikui kuna kitu kimoja hujakijua kuhusu wewe na biashara yako. Inawezekana unatamani sana biashara yako ikue na upate muda wa kufanya mambo mengine unayopenda kwenye maisha, ila bado inakuwa ngumu pamoja na jitihada nyingi unazofanya. Unaweza kufikiri biashara yako haikui kwa sababu unakosa mtaji mkubwa ila sio kweli.

  Leo utajifunza sababu moja kuu ambayo inaizuia biashara yako kukua na kama utachukua hatua baada ya muda utaanza kuona majibu.

  Ili biashara yako ikue ni lazima ukue wewe kwanza. Yaani biashara yako haiwezi kukua kama wewe haukui. Hiyo ndio siri kubwa ya ukuaji wa biashara.

  Unajiuliza unakuaje? Ukuaji ninaozungumzia hapa sio wa maumbile au umri, bali ni ukuaji wa ujuzi na taarifa. Je una ujuzi kiasi gani kuhusu biashara unayofanya? Je una ujuzi kiasi gani kuhusu biashara zingine na miundo ya biashara mbalimbali? Je unapata taarifa sahihi zinazohusiana na biashara kwa muda sahihi? Kama hufanyi vitu hivi ni vigumu sana kwa biashara yako kukua hata kama ungekuwa na mtaji mkubwa kiasi gani.

  Kukua kwako ni lazima na muhimu sana kwa biashara yako. Kuwa na taarifa mbalimbali kuhusu biashara yako, biashara nyingine na maisha kwa ujumla ni muhimu sana. Vitu hivi vitakusaidia kuweza kufanya maamuzi sahihi na pia kuweza kuvuka changamoto mbalimbali unazokutana nazo kwenye maisha ya kila siku. Pia kuwa na ujuzi wa kutosha na taarifa sahihi kuhusu biashara yako kutakusaidia kuweza kuongeza mtaji wa biashara yako.

  Ili kukua pia ni muhimu sana kuangalia imani zetu kuhusu biashara zetu na maisha yetu kwa ujumla. Ni muhimu sana kuwa na mtizamo chanya juu ya biashara yako na maisha kwa ujumla. Kama una imani potofu ama una mtazamo hasi utateseka sana kwa jambo lolote unalolifanya.

  Ili uweze kuwaongoza watu wengine ni lazima uweze kwanza kujiongoza mwenyewe. Na ili kujiongoza mwenyewe ni lazima kuwa na ujuzi na taarifa sahihi kwenye jambo lolote unalofanya. Hii inahusika kwenye biashara, kazi na hata maisha ya kawaida.

  Unawezaje kukua na kuongeza ujuzi na taarifa?

  Ulimwengu wa sasa kujifunza kitu chochote imekuwa ni rahisi sana. Ukiingia kwenye mtandao unaweza kujifunza chochote unachotaka kwa nadharia na hata kwa vitendo. Pia tembelea mtandao wa AMKA MTANZANIA ili kupata mafunzo mbalimbali.

  Pia unaweza kujifunza kwa kujisomea vitabu na hata kusikiliza vitabu vilivyosomwa(AUDIO BOOKS). Weka utaratibu wa kujisomea vitabu na utaona matokeo yake kwenye maisha yako binafsi na kwenye kazi au biashara yako. Kama unataka kuwa unajipatia vitabu vya kujisomea jiunge na mtandao huu kwa kubonyeza maandishi haya.

  Kuhudhuria semina mbalimbali pia kutakusaidia sana kukua na kuwa na mtazamo mzuri juu ya kile unachofanya.

  Tumia kila nafasi ya kujifunza inayokuja mbele yako ili uweze kukua wewe binafsi na kile unachofanya. Kila kitu kinaanza na wewe, wewe ukikua na biashara yako ukikua. Wewe ukibadilika biashara yako pia itabadilika. Ila kama utategemea mabadiliko au kukua kwa kufanya kitu ambacho kila siku unakifanya unajidnganya mwenyewe.